Rais wa Algeria ajitokeza hadharani baada ya mwezi moja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26632-rais_wa_algeria_ajitokeza_hadharani_baada_ya_mwezi_moja
Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mwezi moja na hivyo kuhitimisha uvumi uliokuwa umeenea kuhusu hali yake ya afya.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 20, 2017 11:34 UTC
  • Rais wa Algeria ajitokeza hadharani baada ya mwezi moja

Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mwezi moja na hivyo kuhitimisha uvumi uliokuwa umeenea kuhusu hali yake ya afya.

Bouteflika mwenye umri wa miaka 80, Jumapili alijitokeza mbele ya kamera na kushiriki katika mkutano rasmi. Kulikuwa na uvumi kuhusu hali ya kiafya ya Rais wa Algeria huku wengi wakisema hangeweza tena kuendelea kuingoza nchi hiyo. Bouteflika ameonekana akikutana na waziri wake wa mambo ya kanda ya Maghreb, Umoja wa Afrika, na Jumuiya ya nchi za Kiarabu Abdelkader Messahel.

Katika mkutano huo, Bouteflika amesema kuwa nchi yake bado inakataa nchi za nje kuingilia mambo ya kikanda kama njia ya kufikia suluhisho lolote la mgogoro, kwa kuwa itasababisha vurugu zaidi badala ya kutuliza hali.

Bouteflika alikuwa akipokea ripoti kamili kuhusu hali na maendeleo ya sasa katika kanda za nchi za Kiarabu na Kiafrika, likiwemo eneo la Sahel, na nchi za Mali na Libya.

Algeria imekuwa ikifanya juhudi za kidiplomasia kuimarisha mjadala wa amani na nchi jirani za Libya na Mali, ambazo zimekumbwa na mapigano ya muda mrefu.