Kikosi cha kijeshi cha UN kuingia Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26834-kikosi_cha_kijeshi_cha_un_kuingia_sudan_kusini
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kuingia Sudan Kusini katika kipindi cha chini ya mwezi moja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2017 03:07 UTC
  • Kikosi cha kijeshi cha UN kuingia Sudan Kusini

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kuingia Sudan Kusini katika kipindi cha chini ya mwezi moja.

Kwa mujibu wa Herve Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia oparesheni za kulinda amani na ambaye muda wake unamalizika amesema wanajeshi hao wataanza kuingia Sudan Kusini mwishoni mwa mwezi Aprili na mwanzoni mwa Mei.

Amesema kundi la kwanza la askari hao watatoka nchi za Bangladesh na Nepal na pia kutakuwa na kikosi maalumu cha helikopta kwa ajili ya kulinda amani katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Wanajeshi wengine wa kikosi hicho  cha Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kutoka nchini Ethiopia na wataingia Sudan Kusini mapema mwezi Juni.

Hivi karibuni Ladsous, alitembelea Sudan Kusini na kusema matumizi ya silaha hayawezi kumaliza mgogoro huo.

Aidha aliashiria mazungumzo yake na Rais Salva Kiir wa Sudani Kusini na kusisitiza kuwa mazungumzo ya kisiasa ndiyo njia pekee ya kumaliza machafuko nchini humo.

Aidha amesema, hali ya kiusalama nchini humo inatia wasiwasi mkubwa. Amesema, idadi kubwa ya watu wanaolazimika kukimbia makazi yao kutokana na usalama mdogo, ni onyo kubwa kwa serikali ya Sudan Kusini.