Mripuko wa "Meningitis" waua watu 269 nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27010-mripuko_wa_meningitis_waua_watu_269_nchini_nigeria
Mripuko wa homa ya uti wa mgongo umeua mamia ya watu nchini Nigeria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 29, 2017 09:23 UTC
  • Mripuko wa

Mripuko wa homa ya uti wa mgongo umeua mamia ya watu nchini Nigeria.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Nigeria (NCDC) kimeripoti kuwa, watu wapatao 269 wamepoteza maisha kutoka na ugonjwa huo unaofahamika kwa Kiingereza kama Menengitis katika majimbo 15 kati ya 36 ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya NCDC imeongeza kuwa, kesi 1,828 za ugonjwa huo zimeripotiwa nchini Nigeria katika wiki za hivi karibuni na kuongeza kuwa, kituo hicho kinashirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF kujaribu kudhibiti mripuko wa ugonjwa huo.

Ugonjwa wa Meningitis unaathiri ubongo na uti wa mgongo

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa nchini Nigeria (NCDC) kimebainisha kuwa, homa ya uti wa mgongo iliua watu 33 mwaka uliopita wa 2016, huku wengine zaidi ya elfu 2 wakiaga dunia kutokana na ugonjwa huo mwaka 2009.

Meningitis au homa ya uti wa mgongo ni ugonjwa unaosababishwa na virusi au bakteria, ambapo tishu zinazozunguka ubongo na uti wa mgongo wa muathiriwa huungua na kudhoofika.