Maafisa wawili wa UN waliotekwa nyara Kongo DR, wameuawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27018-maafisa_wawili_wa_un_waliotekwa_nyara_kongo_dr_wameuawa
Imebainika kuwa, maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden waliotekwa nyara katika mkoa wa Kasai katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wiki mbili zilizopita wameuawa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 29, 2017 09:41 UTC
  • Maafisa wawili wa UN waliotekwa nyara Kongo DR, wameuawa

Imebainika kuwa, maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa raia wa Marekani na Sweden waliotekwa nyara katika mkoa wa Kasai katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wiki mbili zilizopita wameuawa.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, maafisa wa umoja huo Michael Sharp wa Marekani na Zahida Katalan wa Sweden wameuawa kishujaa wakijaribu kuchunguza sababu za mgogoro na ukosefu wa usalama Kongo DR, kwa lengo la kuupatia ufumbuzi mzozo wenyenwe na kuwapa amani wananchi wa taifa hilo la Kiafrika.

Gutteres amesema umoja huo utafanya juu chini kuhakikisha kuwa wahusika wa mauji hayo wanafikishwa mbele ya sheria. Amesisitiza kuwa, anatumai serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itafanya uchunguzi wa kina kubaini kiini na wahusika na ukatili huo.

Lambert Mende, msemaji wa serikali ya Kongo DR

Sharp na Katalan walikuwa miongoni mwa wataalamu wa timu ya Umoja wa Mataifa inayochunguza mizozo iliyoiathiri Kongo tangu katikati ya muongo wa 90, wakati vita vya ndani vilipoibua makumi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha na kupelekea kuingia nchini humo majeshi ya nchi sita jirani. 

Lambert Mende, msemaji wa serikali ya Kongo DR amesema kuwa, wataalamu hao wa timu ya Umoja wa Mataifa wakiwa pamoja na raia wanne wa nchi hiyo walitekwa nyara Machi 12 katika daraja moja la Mto Moyo katika mkoa wa Kasai ya Kati, na kupelekwa msituni na wavamizi wasiofahamika. Ameongeza kuwa, mwili wa mmoja wa maafisa hao wa UN ambaye ni mwanamke umepatikana ukiwa umekatwa mikono na miguu.

Wakati huohuo, taarifa ya pamoja ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya imelaani vikali mauaji hayo ya wataalamu wa UN na yale ya makumi ya maafisa wa polisi wa Kongo DR wiki iliyopita.