Upinzani kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais Niger
(last modified Wed, 09 Mar 2016 07:59:53 GMT )
Mar 09, 2016 07:59 UTC
  • Upinzani kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais Niger

Muungano wa upinzani nchini Niger umesema mgombea wake wa kiti cha rais Hama Amadou hatoshiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais dhidi ya Rais Mahamadou Issoufou aliyeko madarakani.

Seini Oumarou, afisa mwandamizi wa muungano huo unaojulikana kama COPA 2016 amesema wameamua kumuondoa Amadou katika uchaguzi huo unaotazamiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu wa Machi, kutokana na sababu kadhaa; ikiwemo mgombea kunyimwa haki ya kufanya kampeni, muda wa kampeni za duru ya pili ya uchaguzi kupunguzwa kutoka siku 21 hadi 10 kinyume cha katiba na madai ya uchakachuaji wa kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais. Hii ni licha ya serikali kushikilia kuwa uchaguzi huo wa Februari 21 ulikua wa huru na haki.

Hama Amadou alitiwa mbaroni katikati ya mwezi Novemba mwaka jana kwa tuhuma za kuhusika katika magendo ya watoto wadogo na hadi sasa anaendelea kushikiliwa katika jela ya mji wa Filingué ulio umbali wa kilometa 180, kaskazini mwa mji mkuu Niamey. Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, tuhuma anazohusishwa nazo ni za kisiasa na kwamba tangu awali serikali ya Rais Mahamadou Issoufou iliamua kumtia ndani ili kumzuia asiweze kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa hivi karibuni, Rais Issoufou alipata asilimia 48.4 huku hasimu wake huyo akipata asilimia 17.7 ya kura zote zilizopigwa na hivyo kushikilia nafasi ya pili.

Tags