Makaburi mengine 13 ya umati yapatikana katikati ya DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27248-makaburi_mengine_13_ya_umati_yapatikana_katikati_ya_drc
Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza habari ya kugunduliwa makaburi mengine mengi ya umati katikati ya nchi hiyo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 03, 2017 22:59 UTC
  • Makaburi mengine 13 ya umati yapatikana katikati ya DRC

Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza habari ya kugunduliwa makaburi mengine mengi ya umati katikati ya nchi hiyo.

José Maria Aranaz alisema jana (Jumatatu) kwamba, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamegundua makaburi 13 mengine ya umati katika mikoa mitatu ya Kasai, Kasai ya Kati na Kasai Mashariki, iliyoko katikati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuripoti habari hiyo kwa maafisa wa serikali.

Amesema, kabla ya hapo pia, kuligunduliwa makaburi mengine 10 ya umati katika mikoa ya Kasai, Kasai ya Kati na Kasai Mashariki, hivyo idadi ya makaburi ya umati yaliyogunduliwa kwenye mikoa hiyo hadi hivi sasa yamefikia 23.

Mauaji ya kiholela dhidi ya raia ni miongoni mwa madhara makubwa ya vita 

 

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema, kuna taarifa za kuweko makaburi mengine ya umati nchini humo. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaendelea na uchunguzi wa kutafuta makaburi zaidi. Hata hivyo amesema, ni kazi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kubaini ni watu wangapi wamezikwa kwenye makaburi hayo ya umati.

Eneo la katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekumbwa na machafuko ya umwagaji wa damu tangu mwezi Septemba 2016 na tangu wakati huo hadi hivi sasa, vikosi vya serikali vinapambana na kundi moja la waasi lililozuka kwenye eneo hilo.