Apr 11, 2017 03:48 UTC
  • Boko Haram wapata pigo jingine kubwa nchini Niger

Afisa mmoja wa masuala ya usalama wa Niger alisema jana kwamba, wanamgambo 57 wa genge la kigaidi la Boko Haram waliuawa Jumapili usiku katika mapigano na wanajeshi wa serikali, kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Mwandishi wa IRIB amemnukuu afisa mmoja wa masuala ya usalama wa Nigeria ambaye hakutaka jina lake litajwe akisema kuwa, mapigano hayo yametokea katika eneo la Gueskérou na kwamba kiongozi mmoja wa Boko Haram ameuawa. Aidha amesema, wanajeshi 10 wa Niger wamejeruhiwa kwenye mapigano hayo.

Mwaka 2009, kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi ya silaha katika maeneo mbalimbali ya Nigeria na mwaka 2015 likapanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon.

Wanajeshi wa Niger katika operesheni ya kupambana na Boko Haram

 

Zaidi ya watu 20 elfu wameshauwa katika nchi hizo nne kutokana na mashambulizi ya Boko Haram tangu mwaka 2009 na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi.

Nchi hizo nne zimeunda kikosi cha pamoja cha kupambana na magaidi wa Boko Haram hata hivyo magaidi hao wanaendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ambapo raia wa kawaida ndio wahanga wakuu wa mashambulio na uvamizi wa genge hilo la wakufurishaji.

Tags