Kuanza maneva ya "Simba wa Afrika" nchini Morocco
(last modified Sat, 22 Apr 2017 11:53:18 GMT )
Apr 22, 2017 11:53 UTC
  • Kuanza maneva ya

Maneva ya kijeshi yaliyopewa jina la "Simba wa Afrika" yameanza katika nchi ya Kiafrika ya Morocco yakishirikisha askari wa Jeshi la Majini la Marekani na wanajeshi 1300 kutoka nchi nyinginen 11.

Maneva hayo ni moja ya mazoezi makubwa zaidi ya pamoja ya kujeshi kuwahi kufanywa barani Afrika kwa kuwashirikisha wanajeshi kutoka Marekani, Morocco, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Uhispania, Canada, Mali, Mauritania, Senegal na Tunisia. 

Maneva hiyo ya kijeshi iliyopewa jina la Simba wa Afrika inajumuisha utoaji mafunzo ya mbinu mbalimbali za oparesheni za kudumisha amani. Mazoezi hayo ya kijeshi yanafanyika huku suala la kurejesha amani likionekana kuwa changamoto kubwa zaidi inayozikabili nchi mbalimbali duniani. 

Maneva ya "Simba wa Afrika" yaanza Morocco 

Katika miaka ya hivi karibuni harakati na hujuma za makundi ya kigaidi zimeongezeka na kuenea katika nchi nyingi za Kiafrika. Oparesheni za kigaidi zinazofanywa na makundi hayo pia zinakwamisha upatikanaji wa amani na utulivu katika aghlabu ya nchi za kiafrika na kuwalazimisha raia kuhajiri na kuelekea katika maeneo mengine ya dunia. Vilevile harakati za makundi hayo za kusajili vijana na wapiganaji wapya katika maeneo mbalimbali imekuwa kengele ya hatari kwa nchi nyingi za Ulaya.

Bara la Afrika siku zote limekuwa likikodolewa jicho la tamaa  na nchi za Magharibi. Nchi nyingi za Kiafrika kwa miaka mingi zilikuwa zikikoloniwa na Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya. Nchi hizo zilizikoloni nchi za Kiafrika kwa miongo kadhaa na kupora maliasili, madini na utajiri adhimu wa nchi hizo, mbali na kuwakandamiza na kufanya jinai za kutisha dhidi ya watu wa Afrika. Pamoja na kuwa aghalabu ya nchi hizo za Magharibi kidhahiri zilionekana zimeondoka barani Afrika baada ya kuanza mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni, lakini kwa mara nyingine tena nchi hizo zimerejea barani humo katika fremu ya siasa za ukoloni mamboleo.

Katika miongo kadhaa ya hivi karibuni nchi za Magharibi zimekuwa zikitumia mwavuli wa masuala kama kutoa misaada ya kijeshi, misaada ya kibinadamu, mikopo ya muda mrefu na kadhalika kwa ajili ya kuendelea kuwepo katika nchi nyingi za Afrika. Marekani pia imekuwa ikitoa zingatio maalumu kwa bara la Afrika katika miongo kadhaa ya karibuni na Washington inachuana na nchi mbalimbali kwa shabaha ya kutaka kuwa na ushawishi mkubwa zaidi barani humo. Washington haitosheki na mahusiano ya kisiasa na kiuchumi na aghlabu ya nchi za bara hilo, bali katika baadhi ya nchi za Afrika kama Djibouti, Marekani imejikita zaidi kwa kuanzisha kambi za kijeshi katika nchi hizo. 

Ukosefu wa amani unaoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Afrika kutokana na kuenea makundi ya kigaidi barani huko umetumiwa kama kisingizio cha nchi za Magharibi ikiwemo Marekani kufanya mazoezi ya kijeshi chini ya mwavuli wa kurejesha amani na utulivu katika nchi za Kiafrika. Hata hivyo hapana shaka kuwa, mazoezi hayo ni wenzo wa kuficha ukoloni mpya wa nchi za Magharibi barani Afrika. Wachambuzi wa mambo wanasema miongoni mwa malengo ya mazoezi hayo ya kijeshi ni kuzifanya nchi za Afrika ziwe tegemezi zaidi kwa nchi za Magharibi kama Marekani na Ufaransa katika masuala ya kijeshi na kiusalama, na vilevile kuziwezesha nchi hizo za kikoloni kupata taarifa za kijeshi na kiusalama za nchi mbalimbali.

 

Harakati za makundi ya kigaidi katika nchi za Kiafrika 

Nchi za Magharibi zinazosimamia mazoezi hayo zinadai kuwa zinalinda na kuimarisha amani barani Afrika, katika hali ambayo nchi hizo zenyewe ndizo chanzo cha migogoro mingi na mivutano inayoshuhudiwa sasa barani humo. Uingiliaji wa nchi hizo katika masuala ya Afrika kama vile kuwepo kwa majeshi ya Ufaransa katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, umesababisha kuibuka mapigano na kuenea hujuma za makundi yenye misimamo ya kufurutu ada. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, miongoni mwa njia za kurejesha amani na usalama katika baadhi ya nchi za Afrika ni nchi hizo za Magharibi kuacha kuingilia masuala ya nchi za kiafrika.

Tags