Viongozi wa kidini Zambia wakosoa kuwekewa mbinyo wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28172-viongozi_wa_kidini_zambia_wakosoa_kuwekewa_mbinyo_wapinzani
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Zambia limekosoa vikali hatua ya serikali ya kumkamata kinara wa upinzani sambamba na kuviminya na kuviwekea mbinyo vyama vya upinzani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2017 23:07 UTC
  • Viongozi wa kidini Zambia wakosoa kuwekewa mbinyo wapinzani

Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Zambia limekosoa vikali hatua ya serikali ya kumkamata kinara wa upinzani sambamba na kuviminya na kuviwekea mbinyo vyama vya upinzani nchini humo.

Askofu Mkuu Telesphore Mpundu, Rais wa baraza hilo amesema vyombo vya usalama nchini humo na hususan jeshi la polisi vinawakandamiza viongozi na wafuasi wa upinzani pamoja na wanaharakati wa nchi hiyo.

Taarifa ya baraza hilo iliyotolewa jana Jumapili imesema: "Tunakosoa vikali mwenendo mbaya unaochukuliwa na viongozi wa chama tawala, wa kuvikandamiza vyama vya upinzani kwa kutumia maafisa wa polisi. Maafisa hao wamekuwa wakitumika kuzuia mikutano na mijumuiko ya wapinzani na vilevile kuwahujumu wakosoaji wa serikali."

Kadhalika viongozi hao wa Kanisa Katoliki nchini Zambia wameeleza kughadhabishwa kwao na hatua ya polisi ya kuvamia makazi ya mkuu wa upinzani nchini humo, mashariki mwa mji mkuu Lusaka na kumdhalilisha kabla ya kumkamata, bila kutoa maelezo yoyote kwa familia yake. 

Rais Lungu wa Zambia (Kulia) na Hakainde Hichilema, Mkuu wa Upinzani

Mapema mwezi huu, polisi nchini Zambia ilimtia mbaroni Hakainde Hichilema, kinara wa chama kikuu cha upinzani cha United Party for National Development UPND, hatua ambayo ililaaniwa vikali na Stephen Katuka, Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hichilema alikamatwa kwa tuhuma za kuzuia msafara wa magari ya Rais Edgar Lungu, magharibi mwa nchi. Tayari kiongozi huyo wa upinzani amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za uhaini, na anatazamiwa kurejea mahakamani wiki ijayo kwa ajili ya kusikiliza kesi dhidi yake.

Aidha Oktoba mwaka jana polisi ya Zambia iliwatia mbaroni Hichilema na Geoffrey Mwamba, naibu kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha UPND kwa tuhuma za uchochezi.