May 01, 2017 07:31 UTC
  • Mamia ya walimu wauawa katika eneo la Ziwa Chad

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umesema kuwa, walimu 600 wameuawa katika eneo la Ziwa Chad kwenye mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram tangu mwaka 2009.

Mtandao wa habari wa Daily Post wa nchini Nigeria umenukuu taarifa iliyotolewa jana na UNICEF ikisema kuwa, mashambulizi ya Boko Haram huko magharibi mwa Afrika yameshaua walimu 600 tangu mwaka 2009 na kupelekea zaidi ya vituo 1,200 vya elimu kufungwa kwenye eneo hilo.

Taarifa ya mfuko huo imeongeza kuwa, kufungwa idadi kubwa ya shule za eneo hilo kumewakosesha neema ya elimu zaidi ya wanafunzi laki moja na 58,900 katika kipindi cha miaka minane iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto wadogo wa eneo la Ziwa Chad ndio wahanga wakuu kiusalama na kielimu wa mashambulizi ya Boko Haram. 

Raia wa kawaida wa eneo la Ziwa Chad ndio wahanga wakuu mashambulizi ya Boko Haram

Watoto wa eneo la Ziwa Chad linalozijumuisha nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad wamepata hasara kubwa kutokana na mashambulizi ya genge la kigaidi la Boko Haram hususan nchini Nigeria.

Neno "Boko Haram" lina maana ya "Elimu za Kimagharibi ni Haram" na kundi hilo la kigaidi lilianzishwa nchini Nigeria mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu za Kimagharibi.

Mwaka 2015 kundi hilo la wakufurishaji lilipanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani na Nigeria yaani za Niger, Chad na Cameroon, suala ambalo limezilazimisha nchi hizo kuunda kikosi cha pamoja cha kijeshi cha kupambana na magaidi hao.

Tags