Maaskofu DRC wamtaka Kabila aruhusu kurejea nchini Katumbi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28624-maaskofu_drc_wamtaka_kabila_aruhusu_kurejea_nchini_katumbi
Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limemuandikia barua Rais Joseph Kabila likimtaka aruhusu kurejea nchini Moise Katumbi, kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
May 04, 2017 07:25 UTC
  • Maaskofu DRC wamtaka Kabila aruhusu kurejea nchini Katumbi

Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limemuandikia barua Rais Joseph Kabila likimtaka aruhusu kurejea nchini Moise Katumbi, kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo.

Katika ripoti ya siri iliyoonekana na shirika la habari la AFP, baraza hilo limemtaka Kabila aruhusu kurejea nchini kutoka uhamishoni mwanasiasa huyo wa upinzani sambamba na kumfutia mashtaka yote yanayomkabili.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kongo DR wamesema katika barua hiyo kuwa, tuhuma dhidi ya Katumbi hazina msingi na zilibuniwa ili kumponda kisiasa bilionea huyo anayemiliki klabu moja ya soka nchini.

Hata hivyo Msemaji wa serikali, Lambert Mende ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, baraza hilo linafaa kuwasilisha mapendekezo na hoja zao kwa mahakama na wala sio kwa Ofisi ya Rais.

Rais Kabila wa DRC

Itakumbukwa kuwa, Mei mwaka jana, mwanasiasa huyo ambaye alitangazwa kuwa mgombea wa kiti cha urais na upinzani katika uchaguzi uliotazamiwa kufanyika Disemba mwaka huo na ambaye anakabiliwa na kesi ya kuajiri mamluki aliruhusiwa kutoka nchini humo na kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi, baada ya kuwekewa vizingiti vingi kwa muda mrefu.

Serikali ya DRC inadai kuwa, Meya huyo wa zamani wa Katanga alihusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya taifa.