Wananchi wa Algeria wajitokeza kuwachagua wawakilishi wao wa Bunge
Wananchi wa Algeria waliotimiza masharti ya kupiga kura, leo Alkhamisi wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwachagua wawakilishi wao wa Bunge lijalo la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Algeria imetangaza kuwa, wapiga kura milioni 23 waliotimiza masharti ya kupiga kura leo walitarajiwa kujitokeza katika vituo vya kupigia kura. Jumla ya wa wagombea 11,334 kutoka vyama 50 wanachuana kuwania viti 462 vya Bunge la Algeria.
Uchaguzi wa leo wa Bunge la Algeria ni duru ya nne tangu Rais Abdelaziz Bouteflika aingie madarakani, na chama tawala cha National Liberation Front (FLN) kinatarajiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo kutokana na udhaifu unaoonekana kwa vyama vya upinzani vya nchi hiyo.
Aidha uchaguzi wa leo wa Bunge nchini Algeria ni wa kwanza tangu bei ya mafuta iporomoke katika soko la dunia na kuwa na taathira hasi kwa uchumi wa nchi hiyo ambayo ni mwanachama wa Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC).
Kadhalika uchaguzi huo ni wa kwanza wa vyama vingi tangu Katiba ya Algeria ifanyiwe marekebisho mwaka jana ambapo kuliingizwa kipengee cha kudhaminiwa uchaguzi huru na wa haki sambamba na kuundwa tume huru ya kusimamia uchaguzi huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Algeria ametangaza kuwa, matokeo ya uchaguzi wa leo wa Bunge yanatarajiwa kutangazwa kesho Ijumaa.