Watu wenye silaha washambulia msafara wa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28884-watu_wenye_silaha_washambulia_msafara_wa_makamu_wa_rais_wa_sudan_kusini
Watu wenye silaha wameushambulia msafara wa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini na kujeruhi walinzi wake watatu ikiwa ni uthibitisho wa wazi kuwa hali ya kiusalama bado ni mbaya nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2017 23:50 UTC
  • Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini
    Taban Deng Gai, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini

Watu wenye silaha wameushambulia msafara wa Makamu wa Rais wa Sudan Kusini na kujeruhi walinzi wake watatu ikiwa ni uthibitisho wa wazi kuwa hali ya kiusalama bado ni mbaya nchini humo.

Press TV imeripoti habari hiyo na kuzinukuu duru rasmi za serikali ya Sudan zikisema kuwa, walinzi watatu wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo, Taban Deng Gai wamejeruhiwa katika shambulio hilo la jana Jumanne.

Taban Deng Gai alijitenga na kundi la waasi mwaka jana baada ya kuahidiwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Salva Kiir. Hata hivyo Waziri wa Habari wa Sudan Kusini amesema kuwa, makamu huyo wa kwanza wa rais wa nchi hiyo hakuwemo kwenye msafara huo kwani aliamua kusafiri kwa ndege.

Msafara huo wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini umeshambuliwa wakati ulipokuwa unaelekea katika mji wa Bor wa kaskazini mwa nchi hiyo ukitokea mji mkuu Juba.

Waasi wa Sudan Kusini

 

Waziri wa Habari wa Sudan Kusini ameongeza kuwa, hakuna mwanajeshi yeyote aliyeuawa na kwamba makamu wa rais amefika salama mjini Bor kwa kutumia ndege.

Sudan Kusini ni nchi changa zaidi duniani. Ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila ya Dinka, kumfuta kazi makamu wake Riek Machar kutoka kabila la Nuer kwa tuhuma za kutaka kumpindua.

Mapigano hayo yameigawa nchi hiyo, yameongeza ugomvi wa kikabila, kusababisha njaa na kuifanya nchi hiyo kuwa na wakimbizi wengi zaidi barani Afrika baada ya wale waliolikumba bara hilo mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda.