Malango: Wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanaendelea kuingia Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28918-malango_wakimbizi_kutoka_sudan_kusini_wanaendelea_kuingia_uganda
Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Uganda amesema kuwa, wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanaendelea kuingia nchini humo kila siku.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2017 22:58 UTC
  • Malango: Wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanaendelea kuingia Uganda

Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Uganda amesema kuwa, wakimbizi kutoka Sudan Kusini wanaendelea kuingia nchini humo kila siku.

Rosa Malango ameeleza kuwa, wakimbizi elfu mbili wa Sudan Kusini huingia kila siku katika nchi ya Uganda na inatarajiwa kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2017 jumla ya wakimbizi laki nne kutoka Sudan Kusini watakuwa wameingia katika nchi hiyo.

Haya yanajiri katika hali ambayo, mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulisema wakimbizi 52,000 raia wa Sudan Kusini waliingia nchini Uganda mwezi wa Januari pekee, kutokana na kuendelea kushuhudiwa mauaji na machafuko katika nchi yao na kubainisha kuwa, watu wanauawa kwa umati na kutendewa jinai nyinginezo za kutisha katika eneo la Kajo-Keji.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Aidha hivi karibuni takriban raia 35 elfu wa Sudan Kusini waliingia nchini Sudan kwa sababu ya ukame na kushadidi machafuko nchini mwao.

Mapigano ya ndani nchini Sudan Kusini yalianza mwaka 2013 kati ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wanamgambo watiifu kwa aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar. Wakati huo Rais Salva Kiir alimtuhumu makamu wake kuwa alifanya jaribio la kuipindua serikali yake. 

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mapigano hayo.