Umoja wa Mataifa: Raia 1,300,000 nchini Niger hawana chakula
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, raia milioni moja na laki tatu katika nchi ya Niger iliyoko magharibi mwa Afrika wamakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN) imetahadharisha kwamba, raia hao ambao ni sawa na asilimia 7 ya raia wote wa Niger wanahitajia msaada wa haraka wa chakula.
Ofisi ya Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imebainisha kwamba, kuna haja ya wananchi hao kupelekewa misaada ya haraka ya dharura ya chakula ili waweze kujikimu na mahitaji ya chakula, na kwamba, endapo hilo halitafanyika kwa wakati kuna uwezekano wa nchi hiyo kukumbwa na maafa ya kibinadamu.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, mbali na Niger kuna nchi kadhaa barani Afrika ambazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Inaelezwa kuwa, mamilioni ya watu wanakabiliwa na tishio la njaa barani humo na kwamba, hali ni mbaya hasa katika mataifa ya Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini, Zimbabwe, baadhi ya maeneo ya Nigeria na eneo la Ukanda wa Ziwa Chad.
Wimbi la ukame limeyakumba maeneo kadhaa ya Afrika kwa miaka kadhaa mtawalia. Hali hiyo imesababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ukame na mafuriko ya mara kwa mara katika nchi nyingi za Afrika yameharibu mazao na ardhi za kilimo na kuwalazimisha mamilioni ya watu kuhama makazi na mashamba yao na kuwa wakimbizi.