Watakaokula mchana Ramadhani visiwani Zanzibar kukiona
(last modified Sat, 20 May 2017 04:17:30 GMT )
May 20, 2017 04:17 UTC
  • Watakaokula mchana Ramadhani visiwani Zanzibar kukiona

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa onyo kwa wananchi watakaokula hadharani katika kipindi cha mchana wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kwamba, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma, Khamis Juma Maalim wakati akijibu swali la mwakilishi wa jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua serikali inatoa tahadhari gani kwa watu watakaobainika kula mchana wakati wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Naibu Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma wa Zanzibar amesema kuwa, utamaduni wa wananchi wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuheshimu kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa makundi yote ikiwemo wa dini tofauti. Alifahamisha kwamba utamaduni huo upo hata kabla ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 wa dini tofauti kuheshimu dini za watu wengine.

Dakta Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar

Alisema kazi ya kutoa elimu kuhusu ujio wa mwezi mtukufu wa Ramadhani imeanza kutolewa na Ofisi ya Mufti ambayo ndiyo yenye jukumu la kushughulikia masuala ya mambo ya dini ya Kiislamu.

Alisema kazi kama hiyo imeanza kutolewa na maimamu wakuu wa misikiti mbalimbali Unguja na Pemba ikiwemo katika Sala za Ijumaa ambazo hukusanya idadi kubwa ya Waislamu kwa wakati mmoja.

Waislamu kote duniani wanatarajiwa kuanza funga ya mwezi Mtukufuku wa Ramadhani wiki ijayo kutegemea na mwandamo wa mwezi.