Wahajiri haramu 4400 waokolewa katika maji ya Mediterranean siku mbili pekee
Duru za habari nchini Libya zimetangaza kuwa kikosi cha gadi ya pwani ya Libya na Italia kimefanikiwa kuokoa karibu wahajiri haramu 400 katika kipindi cha siku mbili kutoka katika maji ya bahari ya Mediterranean.
Taarifa iliyoolewa na kikosi hicho cha gadi imesema kuwa, Alkhamis ya tarehe 18 mwezi huu jumla ya wahajiri 2900 waliokolewa kutoka katika maji ya nchi za Libya na Italia wakati wahajiri hao haramu walipokuwa wakijaribu kuingia nchi barani Ulaya.
Aidha Ijumaa ya jana ya tarehe 19 mwezi huu kikosi hicho cha gadi ya pwani ya Italia kiliokoa jumla ya wahajiri 1500 waliokuwa katika maboti 11 kaika maji ya bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2017 hadi sasa zaidi ya wahajiri elfu 43 wameokolewa katika maji ya bahari hiyo huku wengine zaidi ya 1150 wakiwa wametoweka baharini baada ya boti walizokuwa wanatumia kusafiria kuzama maji.
Kadhalika Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeitaja bahari ya Mediterranean kuwa njia hatari zaidi kwa wahajiri duniani, ambapo njia hiyo hadi sasa imepelekea maelfu ya wahajiri kupoteza maisha. Habari zinasema kuwa, mwaka jana zaidi ya wahajiri 5000 hususan wa Kiafrika walipoteza maisha kwa kuzama baharini katika bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya wanakodhani kwamba watapata maisha mazuri na ajira.