Sudan yaongeza idadi ya askari wake katika mpaka wa pamoja na Libya
Sudan imeanza kutuma askari zaidi katika mpaka wake wa pamoja na Libya katika eneo la Darfur.
Idara ya Habari iliyo karibu na Shirika la Usalama na Intelijinsia la Sudan imemnukuu Liwali wa Darfur Kaskazini Abdul Waahid Yusuf akitangaza kuwa askari zaidi wa vikosi vya jeshi la Sudan wametumwa katika eneo hilo la mpaka wa pamoja na Libya kwa ajili ya kutoa msukumo kwa askari waliotumwa huko.
Yusuf ameongeza kuwa hatua zote zinazohitajika kwa ajili ya tahadhari za kiusalama zimechukuliwa katika maeneo ya mipakani mwa Sudan.
Wakati huo huo Ahmad Khalifa Al-Shami, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Sudan ameeleza kupitia taarifa kwamba vikosi vya harakati za waasi ambao wamekuwa wakipigana vita na serikali tangu mwaka 2003, vimevuka mipaka ya nchi mbili za Libya na Sudan Kusini na kuingia nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo, Muhammad Hamdan, kamanda wa vikosi vya utoaji msukumo na uchukuaji hatua za haraka vyenye mfungamano na makundi ya wanamgambo ametangaza kuwa afisa mmoja wa vikosi hivyo mwenye cheo cha kanali ameuawa katika mapigano yaliyozuka kwenye mpaka wa pamoja wa Sudan na Libya.../