May 24, 2017 07:51 UTC
  • Sudan yaituhumu Misri kuwa inaunga mkono magenge ya waasi

Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir ameituhumu serikali ya Misri kuwa inaunga mkono magenge ya waasi yanayoipiga vita serikali ya Khartoum.

Akihutubia vikosi vya jeshi la nchi hiyo, Bashir amesema vyombo vya usalama vya Sudan vimenasa magari ya Misri yaliyokuwa yakitumiwa na magenge ya waasi katika eneo la Darfur, kusini mwa nchi.

Hata hivyo Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri katika taarifa kwa vyombo vya habari imekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa Cairo inaheshimu uhuru wa kujitawala Sudan na katu haiwezi kuchukua hatua zozote zinazoweza kuvuruga uthabiti wa Sudan au kudhuru wananchi wa taifa hilo.

Hii ni katika hali ambayo, wiki ijayo Ibrahim Ghandour, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan anatazamiwa kuitembelea Cairo, katika safari inayopania kuhuisha uhusiano uliongia doa wa nchi mbili hizo za kaskazini mwa Afrika, hususan mgogoro wa kibiashara ambao ulipelekea kuzuiwa bidhaa za kilimo za nchi hiyo kuingia Misri.

Mwezi uliopita wa Aprili, Sudan iliwasilisha rasmi malalamiko yake kwa Umoja wa Mataifa ikipinga dikrii ya Rais wa Misri kuhusu umiliki wa maeneo ya Hala'ib na Shalatiin, Khartoum ikisisitiza kuwa maeneo hayo ni milki yake na kwamba yameghusubiwa na Misri.

Tags