Waasi washambulia maeneo ya jeshi la DRC
Waasi wanaojiita kwa jina la "Kikosi cha Mapambano ya Wazalendo" wameshambulia maeneo ya jeshi la serikali kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Duru za kuaminika nchini Kongo zimetangaza kuwa, waasi hao wa mkoa wa Ituri wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wameshambulia maeneo ya jeshi la serikali huko Bunga na Alingba na mbali na kuchoma moto maeneo hayo wamepora silaha na mali za wanavijiji.
Habari hizo zimeongeza kuwa, mapigano baina ya waasi hao na jeshi la serikali yamedumu kwa masaa kadhaa.
Kwa mujibu wa habari hizo, Idadi ya waasi ilikuwa kubwa kiasi kwamba wanajeshi wa serikali wamezidiwa nguvu na kukimbia.
Hata hivyo Carlos Kalombo, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkoa wa Ituri amekanusha habari za kukimbia wanajeshi wa serikali na kusisitiza kuwa, jeshi hilo limefanikiwa kuwazidi nguvu waasi na kuzima mashambulizi yao.
Kundi la waasi wa Kikosi cha Mapambano ya Wazalendo lilizuka miaka michache iliyopita katika jimbo la Ituri la kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hadi hivi sasa limeshafanya jinai nyingi dhidi ya raia. Kundi hilo linatuhumiwa pia kufanya mauaji kadhaa ya umati mashariki mwa Kongo.