Waislamu Nigeria watoa sharti la kufika mbele ya tume ya uchunguzi
Waislamu nchini Nigeria wamekataa kufika mbele ya jopo lililobuniwa na serikali ya Abuja kuchunguza mauaji ya Waislamu wa Zaria Disemba mwaka jana, huku wakitoa sharti la kuachiwa huru msomi wa Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakazky ambaye anazuiliwa katika mazingira magumu tangu wakati huo.
Jopo hilo limewapa Waislamu hao hadi Machi 21 kufika mbele yake la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria. Katibu wa jopo hilo Bala Babj amesema zimesalia wiki mbili kati ya wiki 6 walizokuwa wamepewa kuandaa orodha ya mashahidi watakaofika mbele yao kusema wanachokijua kuhusu kadhia hiyo na kwamba wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wamekataa kata kata kujitokeza. Mwenyekiti wa jopo hilo Jaji Muhammad Lawal-Garba amesema tume hiyo itaanza vikao vyake rasmi Machi 21 licha ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini humo kutoa sharti la kuachiwa huru Sheikh Zakzaky. Wananchi wa Nigeria wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakishinikiza kuachiwa huru Sheikh Zakzaky.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 12 Disemba mwaka jana vikosi vya Nigeria vilishambulia marasimu ya kidini ya Waislamu wa Kishia katika mji wa Zaria na kuwatuhumu kuwa walizuia msafara wa mkuu wa jeshi na pia kujaribu kumuua, madai ambayo yamekanushwa na Waislamu hao. Makumi miongoni mwao waliuawa katika hujuma hiyo na wengine wengi wakizuiliwa.