UNSC yatahadharisha kuakhirishwa uchaguzi wa Rais wa Kongo
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewatahadharisha viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuhusu kuakhirisha uchaguzi wa rais wa nchi hiyo na hivyo kuchochea kuendelea machafuko nchini humo.
Jean-Pierre Lacroix Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ulinzi wa amani alisema jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa ajili ya kuchunguza hali ya mambo huko Kongo DR kuwa, hadi sasa taasisi za mpito za kisiasa hazijaundwa huko Kongo katika hali ambayo imesalia chini ya miezi sita hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya ulinzi wa amani amesisitiza pia kwamba idadi ya raia wa Kongo waliolazimika kuwa wakimbizi katika kipindi cha kati ya mwezi Mei hadi Juni imeongezeka kwa asilimia 26; idadi ambayo ni sawa na watu milioni moja na laki tatu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na mgogoro mkubwa uliosababishwa na kuakhirishwa uchaguzi wa rais na vile vile hatua ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo ya kung'ang'ania kubaki madarakani.
Uchaguzi wa Rais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo awali ulipasa kufanyika mwezi Novemba mwaka jana, hata hivyo serikali ya nchi hiyo iliuakhirisha kwa kisingizio cha kukosekana muda wa kuwaandikisha wapiga kura.