Walibya: Saudia inapanga kuasisi utawala wa Kiwahabi nchini kwetu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31774-walibya_saudia_inapanga_kuasisi_utawala_wa_kiwahabi_nchini_kwetu
Raia wa Libya pamoja na wanafikra wa nchi hiyo wameonyesha wasi wasi wao mkubwa juu ya kuwepo viashiria vya kuanzishwa utawala wa Kiwahabi na wa ukandamizaji mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2017 21:58 UTC
  • Walibya: Saudia inapanga kuasisi utawala wa Kiwahabi nchini kwetu

Raia wa Libya pamoja na wanafikra wa nchi hiyo wameonyesha wasi wasi wao mkubwa juu ya kuwepo viashiria vya kuanzishwa utawala wa Kiwahabi na wa ukandamizaji mashariki mwa nchi hiyo.

Walibya sambamba na kubainisha kwamba, vipo viashiria vya kuwepo uwezekano wa kuasisiwa utawala wa Kisalafi wa Kiwahabi kupitia uungaji mkono wa kifedha wa Saudia mashariki mwa nchi hiyo, wamesema kuwa, wanalaani ukandamizaji unaofanywa na Khalifa Haftar, mkuu wa jeshi la Libya katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Khalifa Haftar, mkuu wa jeshi Libya mashariki mwa nchi hiyo anayedaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Saudia na Imarati

Habari zinasema kuwa, makumi ya magazeti yamefungwa, huku waandishi wa habari, wanafikra na wanaharakati wa kisiasa wa mji wa Bengazi, mashariki mwa nchi hiyo wakilazimika kuuhama mji huo kutokana na kutishiwa maisha yao baada ya kuonyesha upinzani wao juu ya mpango huo wa kuanzishwa utawala wa Kiwahabi mjini Benghazi pia namna Khalifa Haftar anavyowakandamiza wakazi wa mji huo. Machafuko na mapigano yalianza kupamba moto mashariki mwa Libya mwanzoni mwa mwaka huu baada ya polisi ya nchi hiyo kusimamisha gari moja aina ya lori lililokuwa limebeba vitabu kutoka Misri, hatua ambayo imekosolewa na wanafikra wa nchi hiyo wanaosema kuwa ni njama za fikra za Kiwahabi za kujaribu kupenyeza mafundisho yao ya kuchupa mipaka na ugaidi nchini mwao.

Jeshi la Libya

Baada ya ukosoaji huo, wanaharakati hao walianza kuandamwa vikali na kulazimika kukimbilia nchi jirani za Misri na Tunisia ili kuokoa maisha yao. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hivi sasa Saudia kwa kushirikiana na Marekani inatumia machafuko ya Libya kupenyeza mafundisho ya Uwahabi ili kutoa fursa na mwanya kwa Marekani na Wamagharibi kutuma majeshi yao zaidi kwa madai ya kupambana na ugaidi.