Mauritania yayatangaza maeneo yanayopakana na Algeria kuwa ya kijeshi
Wizara ya Ulinzi ya Mauritania imeyatangaza maeneo ya mpaka wa kaskazini mwa nchi hiyo ambayo yanapakana na Algeria kuwa maeneo ya kijeshi na kwa msingi huo imewataka raia kutokaribia maeneo hayo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Mauritania imesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko la harakati ya makundi ya kigaidi na magendo na hivyo kuwawia vigumu askari kuwabaini watu wanaojihusisha na harakati hizo zilizo kinyume cha sheria. Kwa mujibu wa ripoti hiyo mtu yeyote atakayeingia katika maeneo tajwa, atakuwa amejiingiza katika hatari ambapo atapigwa risasi bila hata kupewa tahadhari.
Viongozi wa Nouakchott wameyataja maeneo yaliyotajwa kuwa ya kijeshi kuwa ni pamoja na eneo la kaskazini mashariki, kaskazini magharibi, kusini magharibi na kusini mashariki mwa nchi. Hii ikiwa na maana kwamba maeneo yote yanayopakana na Algeria sasa yatakuwa ya kijeshi. Suala la magendo ya binaadamu na uhajiri haramu limeshika kasi zaidi katika miezi ya hivi karibuni na kuzisababishia matatizo makubwa nchi nyingi za Afrika.