Boko Haram yaua Waislamu 22 waliokuwa wakisali msikitini
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria limewaua watu 22 waliokuwa wakisali katika msikiti wa jimbo la Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Afisa mmoja wa idara ya kukabiliana na majanga yasiyotarajiwa katika jimbo hilo na ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa, watu hao wameuawa katika shambulizi la kujiripua lililofanywa na mwanachama mmoja wa genge hilo lenye kufuata mafundisho ya Kiwahabi katikati ya watu waliokuwa wakisali msikitini. Baada ya shambulio hilo, gaidi mwingine aliyekuwa amevalia mada za miripuko alijiripua nje ya msikiti wakati watu walipokuwa wakikimbia kutoka msikitini kuokoa maisha yao. Kwa akali watu 22 wamepoteza maisha eneo la tukio huku wengine 17 wakijeruhiwa na wengine hali zao ni mahututi. Siku chache zilizopita wanachama wa genge hilo lililotangaza kiapo chake kwa kundi la kitakfiri la Daesh, lilifanya shambulizi lingine katika jimbo la Kano kaskazini mwa nchi hiyo na kuua watu watatu na kujeruhi wengine wapatao saba.