Wafanyakazi wa umma DRC waitisha mgomo kutaka nyongeza ya mishahara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32080-wafanyakazi_wa_umma_drc_waitisha_mgomo_kutaka_nyongeza_ya_mishahara
Wafanyakazi wa sekta ya umma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Ijumaa wameitisha mgomo wakitaka serikali iwaongezee mishahara kutokana na ongezeko la gharama za maisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 21, 2017 09:40 UTC
  • Wafanyakazi wa umma DRC waitisha mgomo kutaka nyongeza ya mishahara

Wafanyakazi wa sekta ya umma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Ijumaa wameitisha mgomo wakitaka serikali iwaongezee mishahara kutokana na ongezeko la gharama za maisha.

Faranga ya Kongo imepoteza asilimia 40 ya thamani yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na katika kipindi cha wiki moja iliyopita imezidi kuporomoka kutokana na mgogoro wa kisiasa nchini humo na kushuka bei ya bidhaa ambazo DRC huuza nje ya nchi.

Mfumuko wa bei unatazamiwa kufika asilimia 30 mwaka huu huku mishahara ya wafanyakazi wa umma ikiwa bado haijaongezwa.

Serikali ilikuwa imeafiki kuongeza mishara baada ya mkutano na viongozi wa wafanyakazi lakini bado haijafanya hivyo hadi sasa. Naibu mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Sekta ya Umma Francois Tshimanga ametoa wito kwa wanachama wa jumuiya hiyo kutoka wizara zote kufunga ofisi zao hadi pale malipo ya mishara ya mwezi Julai itakapoongezwa kama ilivyoafikiwa.

Sehemu ya mji mkuu wa DRC, Kinshasa

Haijabainika iwapo wafanyakazi wote wameitikia wito huo lakini Waziri Mkuu Brungo Tshibala amesema atatia saini amri ya nyongeza ya mishhara pale hatua hiyo itakapoidhinishwa na baraza la mawaziri na kisha kutiwa saini na Rais Joseph Kabila.

Matatizo ya kiuchumi Kongo yamezidi kuwa mabaya kutokana na mgogoro wa kisiasa na kuzorota uchumi ambayo yote yana uhusiano na hatua ya Rais Kabila kukataa kuondoka madarakani pale muda wake wa utawala ulipomalizika baada ya miaka 16 madarakani.