Mamia ya maiti za wanachama wa Daesh (ISIS) zimerundikana Libya
Serikali ya Libya imesema mamia ya maiti za wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) raia wa kigeni zimerundikana nchini humo, miezi kadhaa baada ya wapiganaji hao kushindwa na vikosi vya serikali katika mji wa Pwani wa nchi hiyo wa Sirte.
Afisa mmoja wa Kitengo cha Intelijensia nchini Libya ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema miili hiyo imepelekwa katika mji wa Misrata kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba DNA na kufanyiwa utambulisho.
Hata hivyo duru za habari zinasema kuwa, aghalabu ya miili hiyo ni ya raia kutoka nchi za Tunisia, Sudan na Misri.
Vikosi vya Libya vilifanikiwa kuwafurusha wanachama wa genge la Daesh kutoka mji wa Sirte Disemba mwaka jana, mji ambao ulikuwa moja ya ngome za matakfiri hao katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kwa sasa mji wa Benghazi umekuwa uwanja wa mapigano makali baina ya Jeshi la Taifa la Libya na wapiganaji wa Baraza la Mapinduzi la Benghazi lenye uhusiano mkubwa na kundi la kigaidi la Daesh tangu miaka mitatu iliyopita.
Libya ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.