Askari wa gadi ya pwani Libya wawaokoa wahajiri 300
Kikosi cha gadi ya pwani mwa Libya kimetangaza habari ya kuokolewa wahajiri haramu 300 kutoka katika maji ya pwani mwa nchi hiyo.
Ayub Qassim, msemaji wa askari wa majini nchini Libya amesema kuwa, asubuhi ya leo askari wa gadi hiyo wamewaokoa wahajiri 128 karibu na kituo cha kusafishia mafuta cha mji wa Zawiya huku wengine wapatao 150 wakiokolewa katika pwani ya mji wa Sabratha katika maji ya pwani ya magharibi mwa mji wa Tripol.
Wahajiri hao wameokolewa baada ya kuzama ndani ya maji. Sambamba na kuwadia msimu wa joto na kuboreka kwa hali ya bahari, idadi kubwa ya wahajiri wanaokimbia umasikini, hali ngumu na vita na kwa dhana ya kupata maisha bora, wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kufanya safari kuelekea Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean ambayo imegeuka na kuwa kaburi la wahajiri hao.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, karibu wahajiri 2000 wamepoteza maisha yao ndani ya bahari ya Mediterranean.