EU haitatuma timu ya waangalizi wa uchaguzi nchini Angola
(last modified Sat, 29 Jul 2017 02:22:21 GMT )
Jul 29, 2017 02:22 UTC
  • EU haitatuma timu ya waangalizi wa uchaguzi nchini Angola

Umoja wa Ulaya umefuta mpango wa kutuma timu ya waangalizi wake katika uchaguzi wa Angola unaofanyika mwezi ujao, baada ya serikali ya Luanda kutokubali baadhi ya masharti yake.

Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Angola ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, EU imefuta mpango huo wa kutuma waangalizi wake wa uchaguzi katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ghafi, baada ya serikali ya nchi hiyo ya Kiafrika kukataa baadhi ya masharti ya EU, kukiwemo kuruhusiwa kufika katika sehemu zote za nchi wakati wa uchaguzi. Hata hivyo EU imesema yumkini itatuma timu ya wataalamu wake watano wa uchaguzi.

Wizara ya Mambo ya Nje na Tume ya Uchaguzi ya Angola zimekataa kutoa kauli zao kuhusu kadhia hiyo,  licha ya kufahamishwa msimamo huo wa Umoja wa Ulaya.

Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola

Mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola alisaini dikrii inayoidhinisha tarehe 23 Agosti mwaka huu kuwa siku ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.

Dos Santos hata hivyo hatashiriki katika uchaguzi huo na anatazamiwa kuachia ngazi baada ya kuwa rais wa nchi hiyo kwa karibu miongo minne.

Chama tawala nchini humo cha MPLA mwezi Disemba mwaka jana kilimchagua Waziri wa Ulinzi, Joao Lourenco mwenye umri wa miaka 63 kuwa mgombea wa kiti cha urais wa chama hicho.