Machafuko yashika kasi zaidi nchini Burundi
Raia kadhaa wanaripotiwa kuuawa katika machafuko yanayoendelea huko kusini mwa Burundi.
Ripoti zinasema kuwa watu waliokuwa na silaha Jumanne usiku walishambulia na kuua watu watatu katika maeneo ya Makamba na Bururi.
Afisa wa eneo la Makamba, Anicet Niyonzima amesema kuwa mkuu wa zamani wa kijiji cha eneo la Nyagasasa pia ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa njia akirejea nyumbani kwake. Niyonzima amesema serikali inafanya jitihada za kuwatambua na kuwatia nguvuni waliohusika na mashambulizi hayo.
Wakati huo huo mwili wa mlinzi wa shule moja ya eneo la Bururi ulipatika akiwa ameuawa kwa kupigwa risasi.
Mauaji kama hayo pia yameshuhudiwa katika maeneo ya Matana, Mbizi na kadhalika.
Mkuu wa eneo la Makamba amesema watu watatu wametiwa nguvuni katika uchunguzi wa mauaji hayo.
Burundi ilitumbukia katika machafuko ya ndani Aprili mwaka jana baada ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kutangaza kwamba atagombea kiti hicho kwa muhula wa tatu mfululizo.