UN: Mamia ya watu wameuawa katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mamia ya watu wameuawa katika mji wa Kasai ulioko katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia machafuko ya miezi kadhaa katika mji huo.
Ripoti iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, watu wapatao 252 wameuawa kuanzia mwezi Machi hadi Juni mwaka huu, wakiwemo watoto 62 katika mji wa Kasai ulioko katikati mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, vitendo hivyo vya mauaji vimefanywa na maafisa wa serikali, makundi ya wanamgambo au waasi wanaopatikana katika mji huo.
Ripoti hiyo imetolewa na wachunguzi wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa waliopewa jukumu la kufanya uchunguzi kuhusu mauaji dhidi ya raia katika mji wa Kasai ambao katika miezi ya hivi karibuni umeshuhudia machafuko makubwa.
Ripoti hiyo imetolewa zikiwa zimepita siku chache tu baada ya Umoja wa Mataifa kulituhumu kwa njia isiyo ya moja kwa moja jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa lilihusika na mauaji ya umati katika eneo la Kasai.
Tangu mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, watu zaidi ya 3,300 wameuawa huku wengine milioni 1.4 wakilazimika kuyakimbia makazi yao katika mapigano baina ya wanamgambo wanaomuunga mkono Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la waasi katika eneo hilo na askari wa serikali ya nchi hiyo.
Hadi sasa makumi ya makaburi ya umati yamegunduliwa katika mji huo, huku mashirika na asasi mbalimbali za kiraia zikisema kuwa, kumefanyika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika mji wa Kasai.