Jeshi la Algeria lanasa maghala ya silaha za magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32736-jeshi_la_algeria_lanasa_maghala_ya_silaha_za_magaidi
Wizara ya Ulinzi nchini Algeria imetangaza kuwa, imefanikiwa kunasa maghala kadhaa ya silaha yanayomilikiwa na magaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2017 09:01 UTC
  • Jeshi la Algeria lanasa maghala ya silaha za magaidi

Wizara ya Ulinzi nchini Algeria imetangaza kuwa, imefanikiwa kunasa maghala kadhaa ya silaha yanayomilikiwa na magaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, katika operesheni kadhaa za jeshi la nchi hiyo za kukabiliana na ugaidi, askari wa serikali wamegundua maghala kadhaa ya aina 34 za silaha, zaidi ya mada 80 za miripuko, idadi kubwa ya risasi na vyombo vya mawasiliano. Kwa mujibu wa ripoti hiyo maghala hayo yamenaswa katika maeneo ya Medea kusini magharibi, Boumerdès mashariki na Batna, kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Baadhi ya silaha zilizonaswa

Algeria imekuwa ikikabiliwa na hatari ya wimbi la ugaidi kutokana na kupakana na nchi zenye machafuko kama Libya, Mali na Tunisia ambayo nayo imekuwa ikikumbwa na harakati za kigaidi. Polisi na jeshi la Algeria limeimarisha doria hasa kutokana na wasiwasi wa kurejea magaidi kutoka nchini Syria na Iraq na kwenda nchi za eneo la kaskazini mwa Afrika.

Ripoti za kuaminika zinasema, makundi mengi ya kigaidi yanayofanya jinai nchini Iraq, Syria na hata Yemen, yanaundwa na asilimia kubwa ya vijana wanaotoka nchi za eneo la kaskazini mwa Afrika.