Uchaguzi mkuu nchini Kenya
Raia wa Kenya waliotimiza masharti ya kupiga kura Jumanne ya leo wameelekea katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais, madiwani, maseneta, wabunge, magavana na wawakilishi wa wanawake katika uchaguzi ambao unatajwa kuwa na ushindani mkubwa.
Katika uchaguzi wa leo, licha ya kiti cha urais kuwavutia wagombea wanane, lakini mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Rais wa sasa, Uhuru Kenyatta anayetetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha Jubilee, na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye anawania tena kiti hicho lakini mara hii kwa tiketi ya Muungano wa Upinzani wa NASA.
Uchaguzi wa leo umefanyika katika hali ambayo, kumetanda wingu la woga na hofu ya kutokea machafuko, huku ripoti zikisema baadhi ya familia zilishuhudiwa siku chache zilizopita zimeondoka maeneo ya mijini na kuelekea mashambani kwa kuhofia machafuko.
Katika machafuko yaliyozuka mwaka 2008 baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2007 zaidi ya watu 1100 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa. Machafuko hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba, yalikaribia kuitumbukiza nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika vita vya ndani.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) raia zaidi ya milioni 20 waliotimiza masharti ya kupiga kura walitarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa leo.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, ni vigumu kutabiri mshindi wa kiti cha Urais katika uchaguzi huo wa leo wa Kenya hasa kwa kutilia maanani kwamba, uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ulionyesha kwamba, wagombea wawili wa kiti cha urais yaani Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wanakabana koo kwa koo kwa asilimia 50 kwa 50.
Katika kampeni zake za uchaguzi, Rais Kenyatta alisisitiza na kupigia upatu utendaji wake wa awamu ya kwanza hasa katika sekta ya uchumi ambao alisema umestawishwa na kukua sambamba na kuboresha miundo mbinu na mazingira ya ajira na kazi. Rais Uhuru Kenyatta aliwataka Wakenya wampe tena fursa ya uongozi ili akamilishe miradi na mipango aliyoianzisha kwa ajili ya kuboresha maisha ya Wakenya.
Kwa upande wake hasimu mkuu wa kisiasa wa Uhuru Kenyatta, Raila Odinga alisisitiza zaidi katika kampeni zake za uchaguzi juu ya umoja na mshikamano wa kitaifa, vita dhidi ya ufisadi, umasikini na ukosefu wa usalama.
Wapinzani nchini Kenya wamekuwa wakiituhumu serikali ya Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwamba, imeshindwa kukabiliana na ufisadi na ukosefu wa usalama mambo ambayo yameifanya Kenya ikabiliwe na matatizo mengi hasa kudorora kwa sekta ya utalii. Kenya inahesabiwa kuwa miomgoni mwa nchi zenye nafasi muhimu ya kiistaratejia. Pamoja na hayo katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imekabiliwa na matatizo mengi ambapo kubwa zaidi ni suala la ukosefu wa usalama.
Harakati za kundi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia hususan katika maeneo ya mpaka wa Kenya na Somalia zimesababisha mauaji na ukosefu wa usalama katika maeneo hayo. Mbali na suala la ukosefu wa usalama Kenya inakabiliwa pia na mgogoro wa wakimbizi. Mgogoro huo umeifanya serikali ya Kenya itangaze nia yake ya kufunga kambi ya wakimbizi wa Dadaa. Kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni makao ya watu zaidi ya laki tatu na ni kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.
Umasikini, ufisadi na uhaba wa chakula ni matatizo mengine yanayoikabili Kenya kwa sasa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana weledi wa mambo wanasema kuwa, Rais ajae wa Kenya atakabiliwa na kibarua kigumu. Wananchi wa Kenya na wataalamu wa mambo wana matumaini kwamba, kufanyika kwa amani na utulivu kwa uchaguzi wa leo kutaimarisha amani, utulivu na kuimarisha demokrasia katika nchi hiyo na Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla