UN: Pande hasimu Sudan Kusini ziheshimu makubaliano
(last modified Fri, 18 Mar 2016 08:06:47 GMT )
Mar 18, 2016 08:06 UTC
  • UN: Pande hasimu Sudan Kusini ziheshimu makubaliano

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande hasimu nchini Sudan Kusini ziheshimu makubaliano ya amani baina yao.

Baraza hilo limetoa ripoti juu ya wasi wasi wake mkubwa kuhusu hali ya usalama nchini Sudan Kusini na kuzizitaka pande hizo kuheshimu makubaliano hayo ya amani kwa maslahi ya taifa hilo changa barani Afrika. Wajumbe wa baraza hilo wameitaka serikali na wapinzani kuheshimu na makubaliano na wakati huo huo kujiepusha na ukiukaji wa haki za binaadamu hususan ukatili wa kijinsia nchini humo. Ripoti hiyo ya Baraza la Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, serikali ya Juba na wapinzani wake lazima wachukue hatua za dhati za kutekeleza makubaliano hayo ya amani. Itakumbukwa kuwa Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 na kutumbukia katika machafuko mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir Mayardit kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kuwa amepanga njama za kumpindua, suala ambalo lilifuatiwa na vita vya ndani hadi hii leo. Mwezi Oktoba mwaka jana pande hizo hasimu zilitiliana saini makubaliano ya amani ya kusitisha na mauaji baina yao, makubaliano ambayo yanaonekana kubakia tu kwenye makaratasi.