Serikali ya Kenya yajaribu kuyafunga makundi mawili ya haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33188-serikali_ya_kenya_yajaribu_kuyafunga_makundi_mawili_ya_haki_za_binadamu
Serikali ya Kenya inajaribu kulifungia kundi moja la kutetea haki za binadamu na taasisi ya kupigania demokrasia ambazo ziliweka alama ya kuuliza na kuhoji uhalali wa uchaguzi wa Rais uliozusha mzozo ambao ulifanyika wiki iliyopita nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 15, 2017 12:19 UTC
  • Serikali ya Kenya yajaribu kuyafunga makundi mawili ya haki za binadamu

Serikali ya Kenya inajaribu kulifungia kundi moja la kutetea haki za binadamu na taasisi ya kupigania demokrasia ambazo ziliweka alama ya kuuliza na kuhoji uhalali wa uchaguzi wa Rais uliozusha mzozo ambao ulifanyika wiki iliyopita nchini humo.

Hatua hiyo ya serikali ya Kenya ya kutaka kuzifunga taasisi hizo mbili za kutetea haki za binadamu na demokrasia zilizohoji matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita imeibua upinzani na ukosoaji kimataifa.

Barua rasmi zilizoandikwa na bodi ya serikali inayosajili na kusimamia taasisi zisizo za serikali kwa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC) na Kituo cha Utawala Bora (AfriCOG) imesema kuwa, taasisi hizo mbili ziko katika hatari ya kuadhibiwa kwa sababu za kiutawala na zile zinazohusiana na kodi.

Waangalizi wa kimataifa na wa ndani wamesema kuwa, mchakato wa uchaguzi Kenya kwa kiasi kikubwa ulikuwa huru na wa kiadilifu. Hata hivyo kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo NASA, Raila Odinga amepinga matokeo rasmi  ya uchaguzi wa Rais yaliyomtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa kiti cha Urais kwa kwa kumpiku hasimu wake kwa kura milioni 1.4.

Raila Odinga, Kiongozi wa Muungano wa upinzani Kenya (NASA)

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya AfriCOG, Gladwell Otieno amekemea jaribio la serikali ya Kenya la kutaka kufungia taasisi hizo mbili zilizotilia shaka zoezi la uchaguzi wa wiki iliyopita akisema: Hiyo ni hujuma dhidi ya sauti zote huru. 

Wakati huo huo Makundi ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Amnesty International na Zeid Ra'ad al Hussein Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Kenya iheshimu shughuli za taasisi zisizo za serikali NGOs.