Aug 16, 2017 04:27 UTC
  • Watu 27 wauawa katika shambulio la kigaidi kaskazini mashariki mwa Nigeria

Watu 27 wameuawa kaskazini mashariki mwa Nigeria na wengine 83 kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi lililotekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vinaripoti kuwa, shambulio hilo la kigaidi limefanywa na watu watatu akiwemo mwanamke mmoja, ambao walijilipua wenyewe kwenye lango la kuingilia kambi ya wakimbizi katika kijiji cha Konduga karibu na mji wa Maiduguri katika jimbo la Borno, eneo ambalo ni ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haramu.

Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya watu 12 kuuawa kusini mashariki mwa Nigeria na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya watu waliokuwa na silaha kuvamia kanisa moja na kuanza kuwamiminia watu risasi watu waliokuwamo ndani ya kanbisa hilo.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram yanaripotiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni huko kaskazini  mashariki mwa Nigeria maeneo ambayo yanakabiliwa pia na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na ukame na uhaba wa chakula.

Tangu lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009 hadi hivi sasa, genge hilo limeshaua watu wasiopungua 20 elfu na kuwafanya wakimbizi zaidi ya watu milioni mbili na laki sita.  

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari inakosolewa vikali kwa kushindwa kukabiliana na kundi la Boko Haram. Hata kikosi cha pamoja cha nchi za eneo kilichoundwa kwa shabaha ya kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram kinaonekana kushindwa kufikia malengo yake. 

 

Tags