Mar 18, 2016 16:39 UTC
  • Homa ya manjano yaua watu 158 nchini Angola

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza leo kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na homa ya manjano nchini Angola imefikia 158.

Kwa mujibu wa WHO tatizo la ukusanyaji taka nchini Angola ambalo limesababisha kuwepo kwa mirundiko mikubwa ya majaa ya taka katika maeneo ya watu masikini kikiwemo kitongoji cha Viana kilichoko kandakando ya mji mkuu Luanda, na vilevile huduma duni za afya ni miongoni mwa sababu za kuongezeka idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huo.

Kesi ya kwanza ya ugonjwa wa homa ya manjano iliripotiwa mwezi Desemba mwaka jana katika eneo moja la mji wa Luanda ambapo watu wengi waliopatwa na ugonjwa huo unaoenezwa na mbu wanaishi katika eneo hilo.

Tangu miezi kadhaa nyuma, maafisa wa afya wamechukua hatua maalumu za kuanzisha utoaji chanjo kwa wananchi ili kukabiliana na ugonjwa huo unaotibika kwa tabu.

Miongoni mwa dalili za ugonjwa wa homa ya manjano ni maumivu makali ya kichwa, kichefuchefu na kudhoofu kwa mwili.

Kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Angola kasi ya ueneaji wa magonjwa ya malaria, kipindupindu na tumbo sugu la kuharisha pia imeongezeka nchini humo.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa homa ya manjano vinatokea katika bara la Afrika.../

Tags