Watoaji wa huduma za kibinadamu Sudan Kusini waendelea kushambuliwa
Mratibu wa masuala ya kibiadamu nchini Sudan Kusini amesema kuwa mashambulizi dhidi ya watoaji wa huduma za kibiandamu nchini humo yameongezeka.
Serge Tissote amesema kuwa, ongezeko la mashambulizi hayo linatokana na kuendelea kwa vita vya ndani nchini Sudan Kusini ambavyo vinahatarisha maisha ya mamilioni ya raia wa taifa hilo changa zaidi barani Afrika.
Kwa mujibu wa Serge Tissote, mashambulizi endelevu dhidi ya watoaji wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yanaenda sambamba na uporaji wa maghala ya vyakula, madawa na magari yao kama ambavyo baadhi yao pia wameuawa.
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Juba kutoa ulinzi kwa watoaji wa misaada ya kibinadamu nchini humo na kuruhusu watu hao kufanya harakati zao bila ya kizuizi. Hadi sasa watoa huduma za kibinadamu wapatao 82 wameuawa nchini Sudan Kusini tangu mwaka 2013 wakati nchi hiyo ilipotumbukia katika mgogoro na vita vya ndani.
Vita vya ndani Sudan Kusini vimepelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi.