Aug 27, 2017 07:39 UTC
  • Upinzani Angola waitaka tume ya uchaguzi kufafanua matokeo yake

Kinara wa chama kikuu cha upinzani nchini Angola ameitaka tume ya uchaguzi nchini humo kutoa ufafanuzi na maelezo ya kina kuhusu namna ilivyokipa ushindi wa kishindo chama tawala nchini humo.

Isaias Samakuva amesema chama chake cha UNITA kinapinga vikali matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano iliyopita kutokana na uchakachuaji uliofanywa na maafisa wa tume hiyo. 

Amesema matokeo ya Tume ya Uchaguzi Angola CNE, hayaendani na matokeo ya chama hicho kwa kuwa chama hicho kiliendesha zoezi la kujumlisha matokeo ya kura.

Agosti 24, Tume ya Uchaguzi ya Angola ilitangaza matokeo ya awali yaliyoonyesha kuwa, chama tawala cha MPLA kimepata zaidi ya asilimia 64 ya kura na hivyo kuwa mshindi wa uchaguzi huo, huku chama cha UNITA kikitangazwa kuzoa aslimia 26.7 ya kura hizo.

Waliogombea urais Angola

Hii ina maana ya kwamba, mgombea urais wa tiketi ya chama cha MPLA, Joao Lourenco, ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa Angola mwenye uhusiano wa karibu na Rais Jose Eduardo Dos Santos aliyestaafu, ameshinda katika uchaguzi huo. Ushindi wa Joao Lourenco katika uchaguzi wa Angola umemaliza kipindi cha zaidi ya miaka 38 ya uongozi wa Dos Santos. Hata hivyo, Isaias Samakuva amesema kwa sasa taifa hilo halina rais mteule huku Tume ya Uchaguzi ikitazamiwa kutangaza matokeo rasmi na ya mwisho Septemba 6. 

Tags