Kiongozi wa upinzani Zambia: Hatufikirii kulipiza kisasi
Kiongozi wa mrengo wa upinzani huko Zambia jana aliahidi kuwa hana lengo la kulipiza kisasi kufuatia hukumu aliyopewa ya kifungo cha miezi minne jela kwa tuhuma za kutenda jinai.
Hakainde Hichelema ambaye ni kiongozi wa upinzani kutoka chama cha Umoja kwa ajili ya Ustawi wa Taifa amesema kuwa anamsamehe yeyote aliyehusika katika kutiwa kwake mbaroni na kufungwa jela licha ya kutotendewa uadilifu.
Hichelema mwezi Aprili uliopita alikamatwa na kisha kufungwa jela kwa tuhuma za kuzuia kupita msafara wa Rais Edgar Lungu wa Zambia; ambaye kuchaguliwa kwake tena kuwa rais wa nchi hiyo kumekabiliwa na malalamiko ya wapinzani. Baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa hatimaye Mwendesha Mashtaka wa nchi hiyo ametupilia mbali kesi hiyo dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani ambaye alituhumiwa kwa kosa la uhaini la kutaka kuipindua serikali ambalo adhabu yake huko Zambia ni kunyongwa.
Hakainde Hichelema alishindwa na hasimu wake Edgar Lungu katika uchaguzi wa Rais uliofanyika Zambia mwaka uliopita.