Sep 02, 2017 03:03 UTC
  • Boko Haram yaua raia 18 katika mpaka wa Nigeria na Cameroon

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameua watu 18 katika shambulizi lililofanywa kwenye eneo la karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon.

Mauaji hayo yalifanyika jana wakati wanachama wa kundi la Boko Haram waliposhambulia raia kwa kutumia visu katika mji wa Banki ulioko kilomita 130 kusini magharibi mwa Maiduguri, makao kamuu ya jimbo la Borno. 

Mwezi uliopita wa Agosti pia kundi la kigaidi la Boko Haram liliua watu wasiopungua 27 katika maeneo ya vijijini ya Borno. 

Jeshi la Nigeria likiwasaka wapiganaji wa Boko Haram

Wapiganaji wa kundi la Boko Haram wamezidisha mashambulizi na mauaji katika mji wa Maiduguri katika miezi ya hivi karibuni. Kundi hilo linashambulia kwa mabomu misikiti, makoso na kambi za wakimbizi waliokimbia nyumba na makazi yao kutokana na ghasia na machafuko. 

Umoja wa Mataifa umeonya kwamba karibu watu milioni 8.5 katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mashambulizi ya Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Tags