Kiongozi wa upinzani Kenya: Hatutagawana madaraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33908-kiongozi_wa_upinzani_kenya_hatutagawana_madaraka
Raila Odinga kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (NASA) amesema leo kuwa muungano wake hautachangia madaraka, ikiwa zimepita siku mbili baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutengua uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita na kuagiza kufanyika mwingine katika muda wa siku 60.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 03, 2017 09:30 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Kenya: Hatutagawana madaraka

Raila Odinga kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (NASA) amesema leo kuwa muungano wake hautachangia madaraka, ikiwa zimepita siku mbili baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutengua uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita na kuagiza kufanyika mwingine katika muda wa siku 60.

Akizungumza kwa lugha ya Kiswahili nje ya kanisa jijini Nairobi, Raila Odinga amesema kuwa muungano wao hautachangia madaraka na kwamba hawataugawa mkate.  Mahakama ya Juu ya Kenya juzi ilitoa uamuzi kwamba, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC)  haikufuata kanuni na taratibu na kusababisha uchaguzi wa Agosti Nane mwaka huu kutokuwa halali na hivyo kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye alimpita mpinzani wake kwa kura milioni 1.4.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye ushindi wake umetenguliwa na mahakama ya Juu 

Uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ya Kenya umeibua mchuano mpya  kati ya  Kenyatta mwenye miaka 55, na hasimu wake Odinga aliye na miaka 72, huku mivutano ikiongezeka kati ya kambi mbili hizo hasimu. Odinga ambaye mwaka 2007 na 2013 aligombea kiti cha urais,  alirejelea kauli yake baada ya uamuzi huo wa mahakama kwamba wao hawatashiriki katika uchaguzi wa mara ya pili bila ya kufanyiwa marekebisho Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya.