Wito wa serikali ya DRC kwa wapinzani wa kushiriki katika mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33924-wito_wa_serikali_ya_drc_kwa_wapinzani_wa_kushiriki_katika_mazungumzo
Kufuatia kushadidi mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo amewaita wapinzani wa nchi hiyo katika meza ya mazungumzo ili kujaribu kutatua hitilafu zilizoko kati ya pande mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2017 08:17 UTC
  • Wito wa serikali ya DRC kwa wapinzani wa kushiriki katika mazungumzo

Kufuatia kushadidi mgogoro wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo amewaita wapinzani wa nchi hiyo katika meza ya mazungumzo ili kujaribu kutatua hitilafu zilizoko kati ya pande mbili hizo.

Joseph Kapika amewahutubu wapinzani wa serikali ya nchi hiyo akiwaambia kwamba, matatizo na hitilafu zote zilizopo zinaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo.

Waziri wa Uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameashiria maandamano ya utumiaji mabavu katika nchi hiyo na kubainisha kwamba, malengo ya baadhi ya waandamanaji ni kuzusha machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu. Waziri Kapika aidha amewataka wapinzani watupilie mbali mpango wao wa maandamano.

Felix Tshisekedi, kiongozi wa upinzani DRC

Matamshi ya Waziri wa Uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yametolewa katika hali ambayo, mkusanyiko wa amani wa wafuasi wa Felix Tshisekedi Kiongozi wa Muungano wa Upinzani jana uligeuka na kuwa vurugu kubwa. Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo walikuwa wamepanga kufanya mkusanyiko mkubwa wa malalamiko. Hata hivyo serikali ya Kinshasa ilipiga marufuku mkusanyiko huo kwa kile ilichokieleza kuwa ni kuzuia kutokea vurugu na machafuko.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa muda sasa imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa. Mgogoro wa ndani nchini Congo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa Rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila la kusalia madarakani.

Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa Rais mwaka huu, hata hivyo inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa. Wapinzani wanawatuhumu viongozi wa serikali ya Kinshasa hususan Rais Kabila kwamba, wamekiuka vipengee vya makubaliano hayo na kutofanya juhudi zozote za kutekelezwa kwake.

Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kusimamia amani

Jean-Pierre Lacroix Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kusimamia amani alisema hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kwa ajili ya kuchunguza hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba: Umebakia muda mchache kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lakini hadi sasa asasi za kipindi cha mpito katika nchi hiyo hazijaundwa.

Katika hali ambayo wapinzani walikuwa wakitaraji kwamba, hati ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili ingeandaa mazingira ya Rais Kabila kuondoka madarakani, hivi karibuni Kamisheni Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza uwezekano wa kutofanyika uchaguzi katika tarehe iliyopangwa.

Christophe Lutundula mmoja wa wapinzani wa serikali na Naibu kiongozi wa kundi la muungano wa vyama saba vya kisiasa vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema kuwa: Kuakhirishwa uchaguzi kunakiuka Katiba na hati ya makubaliano ya Disemba 31 mwaka jana kati ya serikali na wapinzani.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Sambamba na kupinga hatua hiyo Christophe Lutundula amesema kuwa: Uchaguzi wa Rais hauwezi kufanyika nchini humo madhali serikali ya Rais Joseph Kabila ingali madarakani.

Njama za kuendelea kubakia madarakani kwa kubadilisha Katiba au kwa kutumia njia ya wizi wa kura au kuchakachua matokeo ya uchaguzi ni miongoni mwa daghadagha na wasiwasi wa vyama vingi vya upinzani katika nchi nyingi barani Afrika. Filihali wapinzani wa Rais Kabila wana wasiwasi na mazingira ya kisiasa yanayotawala katika nchi hiyo na wanasema kuwa, kuendelea kuwepo madarakani Rais Kabila ni kinyume na Katiba na ni hatua ambayo inakinzana na mchakato wa demokrasia.

Aidha kutokuweko uhuru wa kisiasa, kupigwa marufuku mikusanyiko na maandamano na wakati huo huo, ukandamizaji wa askari usalama dhidi ya wapinzani ni mambo mengine ambayo yamezidisha wasiwasi mkubwa wa wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 

Hivi sasa mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeingia katika hatua mpya; mgogoro ambao inaonekana unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa mazungumzo na kutekelezwa kivitendo vipengee vya hati ya makubaliano ya mwaka 2016 na hivyo kufanyika uchaguzi wa kisheria katika mazingira ya amani na utulivu, hatua ambayo bila shaka itapelekea demokrasia kuchukua mkondo wake.

Lakini endapo hilo litapuuzwa na kutoheshimiwa misingi ya demokrasia na hati ya makubaliano iliyotiwa saini mwaka jana, basi si jambo lililo mbali kuiona Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikitumbukia tena katika vita na machafuko.