Odinga: Nitashiriki uchaguzi wa marudio Kenya kwa masharti
Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesema muungano wa upinzani wa NASA hautashiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 17 iwapo masharti waliyoyatoa hayatatekelezwa.
Odinga amesema sharti maafisa sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC walioshiriki katika uchakachuaji wa matokeo ya Agosti 8 wapigwe kalamu nyekundu na baadhi yao wafunguliwe mashtaka kwa makosa ya jinai waliyoyafanya.
Odinga amewaambia waandishi wa habari jijini Nairobi hii leo kuwa: "Hatuwezi kuruhusu kosa lililofanyika hapo awali likaririwe tena, hakuna uchaguzi utakaofanyika Oktoba 17 kama ilivyotangaza IEBC, uchaguzi huo ufanyike ima Oktoba 24 au 31."
Matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Kenya uliofanyika tarehe 8 mwezi uliopita wa Agosti, yalifutwa siku ya Ijumaa iliyopita na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo baada ya upande wa upinzani kuwasilisha malalamiko kwamba kulikuwa na uchakachuaji katika mchakato wa kuhesabu kura na kupeperusha matokeo kwa maslahi ya Rais Kenyatta.
Uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ya Kenya umeibua mchuano mpya kati ya Kenyatta ambaye alimpita mpinzani wake Odinga kwa kura milioni 1.4.
Wabunge wa chama tawala cha Jubilee kwa upande wao wamewataka viongozi wa NASA kuheshimu tume za kikatiba na kuruhusu uchaguzi huo ufanyike kama ilivyopangwa na IEBC.
Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, viongozi hao wamesema iwapo upinzani utasusia uchaguzi wa marudio Oktoba 17, basi Rais Kenyatta ataapishwa mara moja kuhudumu muhula wake wa pili.