Ugomvi wa madaraka wapelekea mkuu wa majeshi Lesotho kuuawa
Waziri wa Ulinzi wa Lesotho, Sentje Lebona ametangaza habari ya kuuawa Mkuu wa Majeshi nchini humo, Khoantle Motsomotso baada ya kujiri mapigano kati ya askari walinzi na askari wengine wa serikali ambao walikuwa na ugomvi wa kuwania madaraka.
Kwa mujibu wa Lebona, mbali na Motsomotso askari wengine wawili waliokuwa wakimlinda kiongozi huyo wa kijeshi nao wameuawa na washambuliaji. Habari zaidi zinasema kuwa, mapigano hayo yalitokea kufuatia askari wawili waliokuwa na uhasama na mkuu huyo wa majeshi, kuingia katika ofisi yake iliyopo katika moja ya kambi za kijeshi na kuanza kumshambulia.
Baadhi ya duru za habari zimearifu kwamba, shambulizi hilo lilitokea nyumbani kwake na kwamba askari waliohusika na hujuma hiyo nao waliuawa muda mfupi baadaye. Katika kipindi cha hivi karibuni, Lesotho imekuwa ikishuhudia mgogoro wa madaraka na uingiliaji wa jeshi katika masuala ya kisiasa nchini humo. Kabla ya hapo pia mwaka 2015, Mkuu wa Majeshi wa zamani aliuawa. Lesotho ni nchi ndogo inayopatikana kusini mwa Afrika ambayo tangu ilipopata uhuru imekuwa ikishuhudia mgogoro wa kisiasa.