Misri na Marekani kuanza tena maneva baada ya kusimamishwa kwa miaka 8
Misri imetangaza kuwa itaanza tena kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Marekani baada ya kusimamishwa kwa takriban miaka minane.
Kanali Tamer el-Rifai, msemaji wa Jeshi la Misri amesema nchi mbili hizo zitaanza luteka ya kijeshi ya siku 10 kuanzia Septemba 10.
Cairo na Washington zilianzisha maneva ya kijeshi chini ya kaulimbiu "Nyota Inayong'aa" mwaka 1981 ambayo yalifanywa baada ya kila miaka miwili; hata hivyo mazoezi hayo ya kijeshi yalisimamishwa mwaka 2011 na Rais wa wakati huo wa Marekani, Barack Obama, baada ya kuanza vuguvugu la kumuondoa madarakani mtawala wa Misri wa wakati huo Husni Mubarak.
Itakumbukwa kuwa, Aprili mwaka huu, James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alitembelea Misri kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kijeshi na kiusalama wa nchi hizo mbili.
Hii ni katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Washington ilitangaza kuikatia Misri misaada ya dola milioni 96 za Marekani, kwa madai kuwa serikali ya Cairo ina rekodi mbaya ya ukiukaji wa haki za binadamu sambamba na kuicheleweshea Misri msaada wa kijeshi wa dola milioni 195.
Kila mwaka Marekani imekuwa ikiipatia Misri msaada wa karibu dola bilioni moja na nusu ambapo dola bilioni moja na milioni 300 zinatumika katika masuala ya kijeshi.