Al Shabaab wawaua kwa kuwakata vichwa Wakenya wanne katika Kaunti ya Lamu
Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Al Shabaab la Somalia wamewaua kwa kuwakata vichwa wanaume wanne raia wa Kenya katika mashambulio mawili tofauti waliyofanya katika Kaunti ya Lamu kwenye pwani ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Mashambulio hayo ya leo yamejiri ukiwa umepita mwezi mmoja tangu watu wengine 12 walipouawa huko huko Lamu katika tukio linalofanana na hilo.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu Gilbert Kitiyo amesema mashambulio hayo yamefanyika katika eneo la Silini-Mashambani walikouawa watu watatu kati ya hao wanne ambapo mtu mmoja mwengine aliuliwa katika shambulio lililofanywa kwenye kijiji cha Bobo.
Kwa mujibu wa Kitiyo, washambuliaji wapatao 30 waliojizatiti kwa silaha nzito nzito walivamia nyumba baada ya nyumba huku wakiwaita kwa majina walengwa hao kabla ya kuwatoa kwenye nyumba zao na kuwaua kwa kuwakata vichwa.
Amesema washambuliaji hao walikuwa wamevalia sare za kijeshi huku wamebeba bunduki aina ya AK-47 na kwamba waliwaua kwa kuwakata vichwa wanaume hao wanne kabla ya kutokomea msituni.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu amefafanua kuwa washambuliaji hao walizizingira nyumba zote za wahanga hao kiasi cha kuwafanya washindwe kutoroka.
Msemaji wa operesheni za kijeshi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Al Shabaab Abdiasis Abu Musab amethibitisha kuwa kundi lao ndilo lililohusika na mauaji ya leo ambapo amesema idadi ya waliouliwa ni watu watano na kwamba walengwa hao wote hawakuwa Waislamu.
Mnamo mwezi uliopita wa Agosti pia magaidi wa kundi la kitakfiri la Al Shabaab waliwaua wanaume wanne kwa namna hiyohiyo na pia mwezi Julai wanaume wengine wanane walichinjwa katika vijiji vya karibu.
Wananchi wa Kaunti ya Lamu leo waliandamana na kuchoma moto matairi ya magari kulalamikia hali ya ukosefu wa usalama inayotawala katika eneo hilo. Hata hivyo askari polisi wa kuzuia fujo walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za plastiki kuwatawanya wananchi hao.../