Juhudi za kuunda serikali mpya Libya zinaendelea
-
Mkuu wa Jeshi la Libya, Khalifa Haftar
Baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza kuwa, Khalifa Haftar, mkuu wa jeshi la Libya karibuni hivi ataunda serikali mpya nchini humo.
Mtandao wa habari wa Bawabatul Afriqiyal Ikhbariya (Afrigatenews) umemnukuu Reida El-Oakley, waziri wa afya wa serikali ya Tobruk akisema kuwa, bunge na makundi tofauti ya kisiasa yanaunga mkono kuundwa serikali itakayoongozwa na mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Khalifa Haftar.
El-Oakley ametabiri kuwa, serikali hiyo itakuwa na uungaji mkono mkubwa katika maeneo tofauti ya Libya na itakuwa na nguvu za kudhibiti usalama wa maeneo mengi ya nchi hiyo sambamba na kuyasafisha magenge ya kigaidi yaliyojizatiti katika maeneo tofauti ya Libya.
Waziri wa Afya wa serikali ya Tobruk nchini Libya ameongeza kuwa, serikali itakayoundwa na Jenerali Mstaafu Khalifa Haftar itafanya juhudi kubwa za kurejesha usalama na kuboresha hali ya kiuchumi ya nchi hiyo.
Ikumbukwe kuwa, shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO lilifanya mashambulizi ya kinyama nchini Libya na kuharibu vibaya miundombinu ya nchi hiyo wakati wa kampeni za kumpindua kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Baada ya kupinduliwa Gaddafi na kufanywa uharibifu huo mkubwa, nchi za Magharibi ziliitelekeza Libya na kuacha silaha zimeenea mikononi mwa makundi tofauti yenye ugomvi wa kikabila na kisiasa na tangu wakati huo hadi hivi sasa, Libya haijawahi kuwa na usalama.