Upinzani Kenya: Maafisa wa uchaguzi wametishiwa maisha
Kiongozi wa Muungano wa upinzani Kenya (NASA) Raila Odinga amesema leo kuwa maisha ya baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo yanakabiliwa na tishio kubwa kutoka serikalini kabla ya kufanyika uchaguzi mpya wa rais mwezi ujao.
Odinga ambaye amefanikiwa kuzuia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta mahakamani, amewaambia waandishi wa habari kuwa baadhi ya maafisa wa tume hiyo ya uchaguzi wamepokea baruapepe zinazotishia masiaha yao na kwamba wameondolewa ulinzi.
Odinga amesema kuwa kwa sasa wapinzani wanakabiliwa na hatari kubwa na amemtaka rais Uhuru Kenyatta ajiuzulu. Serikali ya Kenya kwa upande wake haijatoa maelezo yoyote kuhusu madai hayo ya Odinga.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya inakabiliwa na mashinikizo ya wapinzani wanaoitaka ifanye marekebisho baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutengua ushindi wa Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita wakisema kuwa kulikuwa na kasoro katika uchaguzi huo.