Sep 09, 2017 03:22 UTC
  • Shambulio la Boko Haram laua watu wanane kaskazini mashariki mwa Nigeria

Watu wasiopungua wanane wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vinaripoti kuwa, wakulima wanane wameuawa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram kufanya mashambulio katika vijiji vya maeneo ya viunga vya mji wa Maiduguri ambao ni makao makuu ya jimbo la Borno.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wakulima wengi wa maeneo hayo wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya shambulio hilo huko wanamgambo wa Boko Haram wakipora nafaka za wakulima hao.

Ripoti zinaeleza kuwa, maelfu ya wakulima wameyahama makazi yao baada ya kushadidi mashambulio ya Boko Haram katika maeneo mengi ya mji wa Maiduguri katika miezi ya hivi karibuni, hali ambayo imepelekea kusimama shughuli za kilimo na hivyo kuifanya hali ya kibinadamu katika maeneo hayo izidi kuwa mbaya.

Moja ya mashambulio ya mabomu ya Boko Haram katika mji wa Maiduguri

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, karibu watu milioni 8.5 katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mashambulizi ya Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetangaza kuwa watu wasiopungua elfu 20 wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita wamelazimika kuwa wakimbizi kufuatia kujiri mashambulizi na hujuma mbalimbali za kundi la kigaidi la Boko Haram huko Nigeria, Cameroon, Niger na Chad tangu mwaka 2009 hadi sasa. 

Hayo yanajiri huku serikali ya Rais Muhamadu Buhari ikiandamwa na ukosoaji kutokana na kushinda kukabiliana na wanamgambo hao.

Tags